Friday, August 23, 2013

SWAHILI RADIO YAZINDUA APP YA ANDROID PHONES, IPHONE, IPAD,IPOD NA BLACKBERRY

Swahili Radio baada ya kupokea maombi mengi ya wasikilizaji wetu kutoka sehemu mbalimbali duniani, tunapenda kuwatangazia kuwa Radio yetu kwa sasa inapatikana bila mkwaruzo katika simu za viganjani za iPhone, Blackberry, Android phones na katika kila kifaa chenye internet duniani. Endelea Kuangalia Swahili TV na kusikiliza Swahili Radio. Jinsi ya k
utupata 1. Download Tunein (Tunein ni neno moja usiache nafasi) Tunein Radio app kwa simu yako mfano; iphone, ipad,ipod,android au Blackberry 2. Baada ya ku-download , open app na nenda kwenye browser na andika neno swahili radio kisha search. 3. Ukiona logo yetu ya swahili radio bofya na sikiliza.

Tuesday, August 6, 2013

Salim Kikeke? Mfahamu...

Uliyafahamu haya kumhusu Salim Kikeke? Ni mtangazaji mashuhuri wa shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). Je, alifikaje? Na kabla alitokea wapi? Baada ya kumaliza Stashahada ya Umwagiliaji katika Chuo cha Kilimo Nyegezi, Mwanza, alikutana na changamoto kadhaa hasa ya kukosa ajira kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu mfululizo. ”Nilimaliza Stashahada yangu mwaka 1994 kozi ya Umwagiliaji, kwa sasa labda ningekuwa bwana shamba au mfanyakazi wa kilimo,” anasema Kikeke. Baada ya kumaliza chuo, juhudi za kusaka ajira zilikuwa ngumu.Kwa karibu mwaka mzima wa 1995, alikwenda katika machimbo ya Tanzanite ya Mererani Arusha. “Hakukuwa na ajira na kishawishi cha kujiingiza katika uhalifu kilikuwa kikubwa,” anasema bila kueleza zaidi. Katika hatua ya kuepuka mazingira hayo aliamua kuwa ‘Mwanaapolo’ kama wanavyojulikana wachimbaji wa Tanzanite yaani kutumika kuingia kwenye mashimo kubeba mizigo au kazi nyingine migodini. Baada ya kushauriwa na mama yake kuondoka mchimboni, alirejea Dar es Salaam. Katika kipindi hicho Kikeke anasema alikuwa akishinda kijiweni mitaa ya Sinza Kumekucha akiwa na rafiki yake, Joseph Mboya ambaye kwa sasa ni marehemu. Mara baada ya kuona matumaini yakififia kupitia taaluma yake ya kilimo, Kikeke aliamua kubadilisha ukurasa wa maisha baada ya kupiga hodi katika ofisi za kituo cha TV cha CTN ambacho kilikuwa na redio wakati huo ikijulikana kama Classic FM ambayo kwa sasa ni Magic FM. Sababu, nia na ujasiri wa kuchukua uamuzi huo, haikutokea kama ajali, bali ilitokana na ushawishi aliokuwa ameupata kutoka kwa mama yake mzazi ambaye ni marehemu kwa sasa. “Mama yangu alikuwa wa kwanza kunijengea uwezo wa kuingia katika utangazaji, alikuwa anapenda sana kusikiliza habari za redioni na alinishawishi kufuatilia kila habari iliyokuwa inaendelea duniani, nikawa na uwezo wa kutamka maneno vizuri na kusoma habari,” anasema Kikeke. Ilikuwa ni mwishoni mwa 1997, Kikeke alifika katika ofisi za kituo cha kurusha matangazo cha CTN. “Kwa sasa wanaita Magic FM, walikuwa wanafungua kituo kipya cha Classic FM hivyo niliomba kufanya kazi bure, nikapewa kipindi cha kucheza miziki ya Kiingereza,” anasema Kikeke Jambo la kujifunza hapa ni kwamba wakati mwingine katika kusaka ajira, kubali kufanya kazi bila ya malipo, onyesha jitihada zako, huenda ikawa ni njia nzuri ya kuajiriwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo yale ambayo huenda mtu amekwenda kwa ajili ya masomo kwa vitendo. Njia sahihi ya kukaa katika ajira usiyo na ujuzi nayo Anasema baada ya kupata uhakika wa kuendelea na kazi hiyo, Januari mwaka 1998, Kikeke aliamua kwenda kusoma kozi fupi ya Utangazaji habari katika chuo cha uandishi wa habari cha ‘Tanzania School of Journalism (TSJ)’. ”Pale nilisoma cheti kwa miezi mitatu na kurudi tena kazini, nikaanza kusoma habari za kiingereza na Kiswahili wakati mwingine nilikuwa naenda kutafuta habari,” anasema Kikeke. “Hata hivyo mwezi mmoja baadaye wakanifukuza kazi kwa sababu ambazo nisingependa kufafanua zaidi,” anasema. Wakati mwingine hata baya lina uzuri wake Kikeke baada ya kufukuzwa kazi, hakuishia kulia mtaani, badala yake alianzisha mkakati wa kusaka ajira tena kwenye taasisi yenye hadhi ya juu zaidi, Radio Tanzania (RTD) ambayo sasa ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), hiyo ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 1998. ”Kwa kipindi hicho Abdul Ngarawa alikuwa mkurugenzi wa RTD, nikapelekwa idhaa ya Kiingereza, ‘English Service’, na kuandaa vipindi vya muziki kila siku kuanzia saa 12:00 jioni mpaka saa 6:00 usiku,” anasema Kikeke na kufafanua kuwa alikuwa akifanya kazi kwa muda ‘part-time. Alianza kupangiwa vipindi vya kutangaza baada ya kukaa kwa zaidi ya mwaka mmoja. “Baadaye nikapewa kipindi cha Mwelekeo kilichoanzishwa wakati wa maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, nilikuwa mtangazaji wa mwanzoni kabisa katika kipindi hicho,” anasema Kikeke. Katika kipindi hicho, Radio Tanzania walianzisha kituo cha matangazo cha FM, kiitwacho PRT kikitoa matangazo kwa lugha ya Kiingereza. RTD na Kituo cha PRT ndizo kwa sasa zinafahamika kama TBC na TBC1. “Mimi nikaondoka pale na kurudi tena CTN,” anasema. Kurudi CTN Baada ya kurudi katika kituo hicho, Kikeke alifanikiwa kupata nafasi ya kusoma habari kwenye TV mpaka mwezi Agosti wakati kampuni hiyo ilipouzwa na kuwa chini ya kituo cha Channel Ten na DTV. Baadae alihamia ITV. Kuingia ITV/Radio One. Baada ya hapo alifanikiwa kuandika barua ya maombi ya kazi katika Kituo cha Radio One. “Kwa wakati huo Charles Hilary ndiye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Radio One, akaniomba nimpatie mfano (Demo) ya kipindi chochote nilichowahi kufanya, kwa bahati mbaya sikuwa na ya radio ila nikawa na ya TV”, anasema Kikeke. Anaongeza kuwa hali hiyo ikamfanya abadilishe mlango wa kutoka Redio One na kuingia ITV. “Charles Hilary akaipeleka ile demo upande wa televisheni ya ITV, kulikuwa na Betty Mkwasa na Joyce Mhaville, wakaipenda kazi yangu na kuagiza niripoti pale kazini,” anasema. Kikeke alipangiwa jukumu la utangazaji wa vipindi vya taarifa za habari kila siku na habari za ‘Jiji Letu’ hata hivyo mambo yalibadilika kwa muda mfupi pale ofisini. Radio One walikuwa ni Redio washirika wa BBC hivyo walikuwa na mkataba wa kuchukua mtangazaji mmoja kila mwaka na kumpeleka kufanya kazi makao makuu ya BBC kwa muda wa miezi kadhaa. Anasema Mwezi Mei 2003 nikafaulu majaribio ya kuingia BBC, ambako anaendelea hadi leo. Kikeke ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu. Ni baba wa mtoto mmoja ambaye anasoma darasa la saba nchini. “Huku London ninaishi peke yangu,” anasema.
Source: MCL, Tanzania.